Mbunge wa umri mdogo zaidi nchini Kenya amekabidhiwa gari ambalo alikuwa ameahidiwa na Rais Uhuru Kenyatta.
John Paul Mwirigi, 23, ambaye ni mbunge wa Igembe Kusini, takriban kilomita 200 mashariki mwa jiji la Nairobi, alichaguliwa akiwa bado mwanafunzi wa chuo kikuu.
Bw Mwirigi alitumia baiskeli na pikipiki za kusafirisha abiria, maarufu kama bodaboda, kuwafikia watu wakati wa kampeni.
Nyingi za pesa alizotumia wakati wa kampeni alizipokea kutoka kwa wahisani.
Wakati wa kuapishwa, alitumia magari ya uchukuzi wa umma, kufika majengo ya Bunge jijini Nairobi.
Wabunge walipoalikwa ikulu, alipewa lifti na mbunge mwenzake.
Hata hivyo, wakati wa kuondoka, alitumia gari la uchukuzi wa umma maarufu kama matatu.
„Nimetimiza ahadi yangu kwa mbunge kijana wa Igembe Kusini John Paul Mwirigi katika ikulu ndogo ya Sagana," umesema ujumbe kwenye ukurasa wa Facebook wa Rais Kenyatta.
Picha za mbunge huyo akikabidhiwa gari hilo zimepakiwa kwenye ukurasa huo wa Rais.
No comments:
Post a Comment